Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameupongeza Umoja wa waendesha bodaboda Jijini hapa kwa kuchangia mifuko 75 ya sementi kwa ajili ya ujenzi wa wodi  za watoto katika hospitali  ya kanda ya Rufaa  ya Mbeya.
 
Waziri Ummy ametoa pongezi hizo wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi tatu  ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mrundikano wa watoto katika hospitali hiyo “Kwa niaba ya Serikali nawashukuru wadau wote  waliochangia ujenzi huu ila niseme  nimevutiwa sana na mchango wa Umoja wa waendesha Bodaboda kwa kushiriki ujenzi huu, mmefanya jambo jema na la Kizalendo  katika kutatua changamoto za utoaji huduma za afya kwa watoto katika hospitali hii ambayo inahudumia mikoa saba” alisema. Aidha,Waziri Ummy ametoa rai kwa makundi mengine ya kijamii hususan wa kanda ya juu kusini kuiga mfano huo mwema wa bodaboda katika kuchangia  kukamilisha ujenzi huo ili ifikapo  Januari,2017 jengo hilo lianze kutumika.
 
Wakati huohuo Waziri huyo amewaagiza Waganga wakuu wote wa Mkoa na Wilaya  wa hospitali za Umma nchini kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali zilizopo katika maeneo yao ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utoaji huduma za afya  kwa wananchi badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu. “Serikali imedhamiria kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa kanda za juu kusini tumejipanga kuhakikisha kuwa ujenzi wa jengo la uchunguzi (Diognistic Centre) lililokwama kwa takribani miaka saba  unakamilika ndani ya  mwaka mmoja”,hii itawaondolea kero wananchi wa nyanda hii kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya huduma za vipimo vya kiuchunguzi wa magonjwa kama TC Scan Kuhusu matibabu ya saratani kwa njia ya dawa (Chemotherapy Waziri Ummy alisema matibabu hayo yataanza kutolewa mapema mwakani na hivyo itapunguza kero kwa wananchi wa kanda ya Mbeya kwenda katika hospitali ya saratani ya Ocean Road.
 
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya, Dkt. Godlove  Mbwanji alisema ujenzi wa wodi  hizo ambao utagharimu shilingi milioni 300 ambazo zinatokana na fedha za ndani za hospitali hiyo pamoja na michango ya wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mbeya.Jengo hilo litakuwa na vitanda 76 na hivyo kumaliza kabisa tatizo la wagonjwa kulala chini. Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya inahudumia mikoa ya Iringa,Njombe,Songwe,Katavi,Ruvuma,Rukwa Iringa pamoja na Mbeya.
 
Picha za matukio ya uwekaji wa hiwe la msingi la ujenzi wa wodi tatu za watoto mjini mbeya
 
 
 
 
 

Feature News & Events

Go to top