Customer Feedback Centre

Ministry of Health

PUUZENI TAARIFA ZA UPOTOSHAJI WA CHANJO YA HPV.

Posted on: April 22nd, 2024Na WAF – Mtwara.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa huo kuepuka na kupuuza taarifa zozote za upotoshaji kuhusiana na Dozi moja ya Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa mabinti wenye umri wa Miaka tisa hadi kumi na nne.

Ameyasema hayo Aprili 22, 2024 wakati akizindua Kampeni ya Dozi moja ya Chanjo ya HPV kwa mabinti Wenye umri wa Miaka Tisa hadi Kumi na Nne katika viwanja vya shule ya sekondari ya Mustafa Sabodo Mkoani Mtwara.

“Chanjo hizi ni salama kwa watoto wetu kama ilivyothibitishwa na wizara ya afya kwa kushirikiana na shirika la afya duniani WHO, hivyo tupuuze taarifa zozote zitakazojitokeza za kusema chanjo hzi zinamadhara”

Kanali Sawala amewata watoa huduma za chanjo kuimarisha usimamizi na utoaji huduma za chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi na kutoa majibu ya kitaalam pale inapotokea taarifa za upotoshaji kwa jamii.

“Kuna watu watajitokeza na kutoa taarifa za kupotosha jamii juu ya chanjo hii hivyo niwasihi kuzipuuza taarifa hizo wasikilizeni wataalamu pindi linapotokea hilo haraka nendeni mkatoe taarifa sahihi kwa wananchi ili kuepusha upotoshaji”

Kanali Sawala amesema serikali itaendelea kuimarisha huduma ya chanjo zinazotolewa na kutoa elimu kwa jamii juu ya masuala mazima ya afya na kuwata wazazi, walezi na waalimu kusimamia zoezi la utoaji wa chanjo mashuleni na kuwahimiza mabinti hao kupatiwa chanjo hiyo.

“Mkoa wa Mtwara unatarajia kuchanja wasichana takribani laki moja na nimatumaini yangu kwamba mabinti hawa wote watafikiwa na kuchanjwa na kufikia lengo la chanjo hii.

Amesema Ili mabinti zetu wanufaike na chanjo ya HPV tunaowajibu wa kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwahimiza kujitokeza kupata chanjo hii zinazotolewa katika shule za msingi na sekondari na vituo vilivyotengwa vya kutolea huduma ya afya nchini “. Ameeleza Kanali Sawala